Short StoriesWritings

Khawaatwir (Hadithi fupi)

By November 26, 2020 1,268 Comments

Khawaatwir (Hadithi fupi)

Katika maisha, kila mja huwa na shughuli zake anuwai, na kila adinasi yuko na sifa alizosheheni. Na sifa ndizo chanzo kikuu ambacho humfanya mtu kupendwa ama kuchukiwa. Nami sikujua kama nilikuwa wa mapenzi ama chuki. Lakini pia kuna jambo ambalo sikuwahi liajabia abadan katan. Kusemwa, nilielewa fika kuwa maneno ni kama kivuli nacho kitakufwata kila uendako, na heri kivuli shamsi likizama huondoka. Maneno hukufwata hadi kaburini. Mathalan, ukiwa mchafu utaambiwa unanuka, ukiwa safi, utaambiwa unaringa. Wanaadamu hawaachi kukuchamba. Mwanaadamu…

Basi siku ya kwenda mjini ilifika. Sikuwa na uwezo wa kuabiri gari, basi kama ujuavyo kuwa mtu hujikuna ajipatapo, na kwa kukosa budi, nilianza guu mosi guu pili kichwani nina tafakuri. Nilikuwa na shughuli zilizoniandisi. Nilihitaji kwenda mjini kupatana na wanaume kadhaa wa kutoka bara ili niwaeleze jinsi ya kuishi duniani. Wabara, ndio wabara. Na kusema mbara simaanishi ati nimezama na kupotea katika ukiritimba na ukabila. Ninamaanisha kusanyiko la adinasi, lufufu ya wanaadamu katika sehemu mbali na bahari. Sehemu inayojulikana kukosa hari ya eneo na kuwa na hari ya nyoyo. Na kaida ya maisha si kutafutana, ni kutafuta. Katika mwendo wa dakika ishirini hivi na vichopo juu, nilikuwa nimefika kwenye daraja. Hapo nilikumbana na rijali mmoja akiwa amebeba rundo la karitasi mikononi. Sadfa yetu hii bado naikumbuka hadi sasa. Ilinipa upeo ambao hapo mwanzo ulikuwaumejitanibu nami kama mbingu na ardhi. Upeo kuhusu waandishi na wachapishaji nani. Kuhusu subira ndio nini katika mustakabali wa waandishi. Basi katika mazungumzo yetu, alinitajia kijana mmoja ambaye alikuwa amesheheni sifa si kidogo. Na hivi ndivyo tulivyoanza mazungumzo, ambayo yalikuwa kama chane, nao mwanzo wa chane ni chane mbili.
‘Za masiku?’ Alianza kama tushawahi kutana.
‘Nzuri, sijui za utokako?’ nikamjibu kama nilikuwa namjua. Nilipomtazama wajihi, nilikuwa simjui hata kwa ahlan wa sahlan.
‘Mbona unaharakisha kama umechelewa.’
‘ la niko na amana nawapelekea watu kadhaa, wala si kadha wa kadha. Haiyamkiniki kuwa kuna wanaadamu katika hii dunia wanathamini darahimu kuliko uanadamu. Pesa imekuwa wazimu kwao. Nashindwa kustahamili pesa ni nini haswa? Mbona mtu awe na roho kama hiyo..’ akanikatisha. ‘Lo, umegonga ndipo. Unaongea kama mwandishi Izirare, katika kitabu chake cha Ndoto. Maneno hayo hayo aliakemea. Huyu kijana ukisoma dibaji ya kitabu chake waeza usisome kitabu hicho. Maana amejidunisha mno, nakumbuka kuna mstari aliandika akisema, mimi ni kijana mdogo sana katika ulingo wa waandishi. Tajriba yangu ni ndogo sana katika kuyaelewa maisha. Kwa hivyoukitaka kunisoma, soma ujuwe hutapata unayoyadhania, mimi bado nahitaji mtu wa kunishika mkono nisije nikakungwaa. Na ukiridhika na mkono wangu katika kudariji na kuimbua lugha kwa fasaha, basi usinivishe joho ambalo lanipwaya, sema mashaallah, Mungu amzidishie. Ukiona nimekosea, nirekebishe. Na kusema Mimi simaanishi mimi ya maana, namaanisha mimi ya kiswahili. Maana mimi ndio mwanzo wa kiburi, taraghani, ushabaki na ghera.Na huyo ndio Izirare Ahmad.’

NilIyasikiza yale maneno kwa makini. Yalikuwa si maneno ya kawaida, mathalan, nilielewa kuwa kuna maneno yasioingia akilini na yasiyoingia kwa akili, haya yalikosa mahala pa kuyaweka. Maana mwanzo ni mwandishi, ni waandishi wangapi hupiga jeki kujianika kama vile mahindi yanavyoanikwa ugani yapate nishati. Hujianika, hapa nieleweke vyema, kujianika ni tofauti na kujistawi. La kuanikwa huondolewa baadaye jua linapozama, linalostawi huwa pale kwa ayami baada ya ayami. Nalo huyu Izirare hakua nalo. Tena nakumbuka yule rijali alisema ananigusia tu kuhusu huyu mwandishi. Hamu na ghamu iliniparamia kutaka kuonana naye, angaa nipate kumuona ni kijana wa dini gani, ama ana mustakabali gani wa maisha.

Yule rijali aliona hamu niliyokuwa nayo kutaka kumjua huyu kijana. Magari yalikuwa yanatupita kwa mwendo wa kasi sana, upepo wake ulitatiza macho yetu, hata yakawa yanalenga lenga machozi. Yule kijana aling’ang’ana na karatasi zake zisije zikabebwa na upepo, si upepo wa magari, si upepo wa mwezi wa julai, si upepo wa bahari juu ya daraja, upepo, upepo wa nakama. Watu walitupita bila salamu, maana salamu ni kwa unaemjua, usiyemjua humthamini. Nikamwambia anieleze vizuri kuhusu Izraeli. Alicheka sana, sikujua kama ni kwa vile nililitamka jina lake vibaya. Lilikuwa jina gumu kwa haki. Sijawahi lisikia mie. Nilihitaji mazoezi angaa. ‘Ni Izirare. Huyu kijana, hana elimu ya fasihi isipokuwa ile yenye ameisoma kwa vitabu vya fasihi andishi, vitabu vya waandishi, si mzuri wa lugha katika uandishi, lakini ana umbuji wa aina yake. Lugha ime.kubali mashaallah, akiongea utadhani mwendawazimu kwa anayoongea kwa sababu hayataingia akilini mwako. Ni mtu anayechambua maisha kwa aina yake, mathalan anasema, ukitaka kuwa mkweli anayependwa, kuwa muongo zaidi, utapendwa, sifu asiyestahili sifa, utapendwa. Macho yako yasione mabaya, yaone tu mazuri. Anasema hakuna anopenda pesa, isipokuwa watu huthamini chenye pesa inaeza nunua. La mwisho akaamba kuwa ati mwendawazimu wa mapenzi anajua maisha kuliko yoyote yule. Huyo ndio mwaandishi.’

Lo! Nilimaka. Kumbe kuna mengi nilikuwa siyajui, mwendawazimu wa mapenzi ndio, lo. Kumbe mimi ni mjinga kiasi hichi. Kuna mabo yamenifutu, siyajui utandu wala ukoko. Maisha ni mukhtasari wa barua ambao wino wake haujulikani, wala lugha yake vile vile haijulikani. Nilitaka kupata habari zaidi kuhusu huyu mwandishi. Kadri nilivyoelezewa ndivyo hamu yangu ilikuwa kama tiara inapeperushwa na upepo. Ilikuwa inapepea juu kwa juu. Hata niliogopea kupatwa na cheleo. Nilipoangalia mbele, niliona palikuwa na makutano, njia ya msalaba ambayo katika mwambao wa pwani, washirikina hupatumia kumwaga mangojwa kwa njia ya pesa. Waokotaje wanahabari zaidi maana mvua imewanyea bila shaka. Njia moja ilitoka upande wa mkono wa yamini nyingine ilitoka upande wa shemali. Rijali alikuwa aingile na ile ya shemali. Mimi ilifaa ninyoshe moja kwa moja hadi makadara. Makadara palikuwa na uwanja mkubwa. Shughuli iliyoniambaa haikuwa ndogo, ilikuwa shughuli ya ndovu kula mwanawe, utawapata waswahili wenyewe wakikuambia kuwa ilikuwa babu kubwa.

Nikashindwa kuagana naye ili tuachane, nikaandamana naye. Nikamwambia ingekuwa aula zaidi anieleze kuhusu kijana huyo mraufu. Akaniambia kuwa kuna kitabu chake kingine kinaitwa Mlangoni. Hiki kitabu chake kimebeba khawaatwir nyingi sana. Akisema mlangoni alimaanisha mlango wa kaburi, mtu mwenye yuko katika kuikata roho analia akihuzunika kuhusu aliyoyafanya duniani akisema kumbe dunia ni kama mti wa kivuli, unapumzika kidogo kisha utaiacha. Mti wa kivu hufikia wakati matawi yamekauka,miale ya jua lapenyeza. Kisha, mtu afapo ndipo hugundua mengi, ndipo huamka na kuona, kila alichokiita chake anakiacha, si mke wake, nyumba yake, pesa zake, watoto wake. Anaenda hana kitu. Ndipo huamka katika ndoto, maana ndipo hujua kuwa alichotumia ndio afaa kukiita chake. Hiki kingine asaidie kila mwenye hana, asiwe mchoyo na chakula maana chakula kimeua watu. Asiwe bahili maana pesa pia imeua wengi, haina thamani ila hasara tu, aikosane na majirani kwa mkewe maana akifa, majirani ndio msaada. Akamalizia akanena kuwa, nusu ya hasara yawanaadamu duniani ni kuwa hawatumii vipawa vyao, ila maumbile hayakuwa bahili katika kuvigawa vipawa.

Nilishikwa na hamu kujua alikuwa dini gani. Nilipouliza, nikaambiwa hajajiweka wazi na kumjua kwake ni kama kuunga moja na moja uzidishe na moja halafu ugawanye na mbili. Ameandika kitabu kingine akakiita Maisha Sebuleni. Hiki ameandika kwa minajili ya rafikiye, huyu rafikiye alikuwa abamwiita mwislamu nusu, maana kichwa cha mwandishi huyo kukipata na walai, kofia ni mwiko, unaeza kuwa naye mwaongea na watu wanaswali, pia inaeza kuwa hivyo wakati watu wanasali. Huwezi mgundua kwa urahisi, ni msiri mkubwa, hufanya mambo yake kwa siri sana, labda umsome ndo utamwelewa angaa kwa nukta mbili au tatu. Kabila lake limenifutu kabisa kumjua, wako wanaosema anatoka bongo kwa ufanisi wa lugha na jina lake, wako wanaosema ni miongoni mwa mijikenda, wapo wanaosema alitoka milima ya taita, kwa hivyo imeniwia vigumu kujua. Na bado hutunga tungo adhimu ambazo huzipenda sana.
‘kama gani?’ nikauliza.
‘Kitabu alichoandika cha tungo amekiita Mashairi Ya Nairobi. Tungo zilizohumo kuzielewa ni kama kukata jongoo na meno, utadhani walengwa si wa Nairobi, niliopata kuilewa kidogo ni hii,

jabari kahasirika,kalemaa mapumbu
amekuwa mwathirika, kanyamaza mbumbumbu
Hatambi mwenda hakika, wanampiga kumbu.’

‘Hapa jabari utadhani ni Mola, ila kaanza kwa herufi ndogo, akimaanisha kiswahili, kiswahili nairobi kapewa lahaja yake, mwanzo wandishi huyo katika kurasa zingine kwa njia ya ushairi akariri kwa ari na akijidhihiri kughuriwa na lugha hiyo akidhani lahaja ya nairobi. Kumbe ndivyo lugha ya huko huzungumzwa. Kwa sababu yeye ashiki wa lugha, akaitungia tungo zake na walengwa hawashughuliki kusoma. Haiyamkiniki aliyezoea tambuu kutumia tumbaku, haiwezi.’ Nilikuwa nimetosheka nikaelekea mahali nilikuwa nikienda. Muda wa saa nne kamili nilikuwa nimefika Makadara. Hapakuwa na isimu ya mtu hata mmoja. Hata wauzao mihogo niliowazoea kuwaona pale, waliadimika kama kaburi la baniani. Nilipigwa na butwaanikabaki nikitia na kutoa. Sharuti pawe na jambo. Nikakiri. Nilisikiwa nimeingiwa na woga. Mara anga likapiga umweso mkubwa uliofwatana na radi. Mara mvua ikaanza kunyesha. Jinsi mawingu yalivyokambana sikupata kujua. Mvua inanyesha si haba. Nikatafuta mahali nikajikingama mvua.

Katika harakati zile, nikaona kijana akipita katika mvua ile pasi kujikinga katika veranda. Nikashindwa kwani alikuwa bahaimu ama razini. Mtu asiyejua heri kinga kuliko tiba. Nikapaaza sauti kumwiita. Akaniangalia akafwata shughuli yake. Nikamwiita kwa nguvu zidi, ‘ewe ghulamu.’ Akanitazama, akawa anataka kwenda akasimama akwaza mwanzo. Akapura pura kidevu chake kisha akaja. Alipofika karibu, nikamuona kama alikuwa izirare Yule kijana niliye hadithiwa. Naye pia mkononi alikuwa na karitasi katika bahasha. Yalikuwa yametota si haba. Nikanyosha mkono kumsalimia ila hakuupokea. Nilishtuka ghaya ya kushtuka .

By Izirare Hamadi

1,268 Comments